Kiwango cha ukimbizi wa ndani CAR kinatisha- UNHCR

23 Januari 2018

Idadi ya wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR sasa imefikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu kuanza kwa mzozo nchini humo mwaka 2013.

Idadi ya wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR sasa imefikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu kuanza kwa mzozo nchini humo mwaka 2013.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watu Laki Sita na elfu themanini na nane walikuwa ni wakimbizi wa ndani hadi disemba mwaka jana, kiwango ambacho ni ongezeko kwa asilimia 60 ikilinganishwa na mwaka 2016.

Sababu kuu ni kuongezeka kwa mapigano nchini CAR hususan eneo la kaskazini-magharibi mwa nchi ambapo msemaji wa UNHCR Adrian Edwards anasema

(Sauti ya Adrian Edwards)

“Idadi ya raia waliokimbilia nchi jirani nayo imefikia zaidi ya laki tano na elfu arobaini na mbili, hii nayo imeongezeka kwa asilimia 12 ikilinganishwa na mwaka 2016. Kwa nchi ambayo idadi ya raia wake inakadiriwa kuwa milioni 4.6, takwimu hizi mbili zikiunganishwa zinawasilisha viwango vya juu zaidi vya machungu na watu wenye uhitaji.”

UNHCR inasema mahitaji yanaongezeka kutokana na ghasia kufurusha watu, magonjwa nayo kama vile Malaria, kipindupindu na magonjwa ya njia ya hewa.

Hata hivyo Bwana Edwards anasema idadi ya wenye uhitaji inaweza kuwa kubwa zaidi kwa sababu ukosefu wa usalama unasabisha washindwe kufika baadhi ya maeneo ambako watu wamejificha.

Amesema UNHCR inasambaza huduma muhimu kwa wakimbizi wa ndani na inashirikiana na wadau wake kujenga makazi ya mapya ya kuwahifadhi wakimbizi.

Msemaji huyo ameonya kuwa iwapo wakimbizi watashindwa kurejea makwao ndani ya miezi michache ijayo, basi wana wasiwasi vijiji vilivyokumbwa na mapigano vitashindwa kushiriki upanzi wa mazao na hivyo kusababisha ukosefu wa chakula baadaye mwaka huu.

Mwaka huu UNHCR inahitaji dola milioni 176 ili kukidhi operesheni zake huko CAR, wakati huu ambapo hata ombi la mwaka jana la dola milioni 209 lilifadhiliwa kwa asilimia 12 pekee.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud