Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 1.6 zahitajika Somalia kuokoa mamilioni ya watu: OCHA

Mwanamke Msomalia anampa mtoto maji katika kituo cha Usajili kwa ajili ya ya Misaada. Picha: OCHA/Giles Clarke

Dola bilioni 1.6 zahitajika Somalia kuokoa mamilioni ya watu: OCHA

Ombi maalumu la dola zaidi ya bilioni moja limetolewa leo nchini Somalia na mratibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA kwa ajili ya msaada wa kuokoa maisha ya mamilioni ya watu mwaka huu wa 2018. Selina Jerobon na tarifa kamili

(TAARIFA YA SELINA JEROBON)

Akizindua ombi hilo mjini Moghadishu la dola milioni 1.6 kwa ajili ya mipango ya kukabiliana na mahitaji ya haraka ya kibinadamu kwa watu milioni 5.4 mwaka huu, mratibu huyo Peter de Clercq amesema  suluhu ya muda mrefu ya ukame, vita na watu kutawanywa bado ni changamoto kubwa na jitihada za ziada zinahitajika ili kuepusha tishio la baa la nja na kurejea kwa majanga mengine nchini Somalia.

Amesisitiza kwa wakati huu ni lazima kushughulikia mahitaji ya haraka ya kibinadamu na wakati huohuo serikali ya Somalia, Umoja wa mataifa na jumuiya ya kimataifa kusaka suluhu ya muda mrefu ya mgogoro wa Somalia.

Ameonya kwamba ukata unatishia mustakhbali wa mamilioni ya watu, na wasipoendelea kuokoa maisha sambamba na kuwajengea uwezo watu wa taifa hilo la pembe ya Afrika baa la njaa litakuwa limecheleweshwa na sio kuepukwa.

Amesema kipaumbele cha OCHA mwaka 2018 kwa Somalia ni kuhakikisha wanaepuka baa la njaa nchini humo hasa ukizingatia kwamba watoto milioni 1.2 wanakadiriwa kukumbwa na utapiamlo 2018 huku 232, 000 kati yao kukabiliwa na unyafuzi.