Baada ya mwaka sasa msaada wafikia jamii Wau:IOM

Raia wa Sudan Kusini hususan waishio kusini mwa mji wa Wau wameanza tena kupata msaada mwaka moja baada ya mawasiliano kukatwa katika eneo hilo kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Flora Nducha na taarifa kamili
(TAARIFA YA FLORA)
Kwa muda wa mwezi mmoja sasa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limefanikiwa kurejelea utoaji msaada wa huduma za kiafya kwenye eneo la Greater Baggari, lilioko kusini mwa mji wa Wau. Eneo hili lilikuwa halifikiki kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja. Sasa kutokana na kuwepo mwanya wa kufika maeneo hayo , miezi kadha iliopita , shirika la IOM limeweza kuwafikia na kuwapa msaada watu waishio mbali na maeneo hayo.
Misaada ya kiutu katika eneo la Baggari, ilisitishwa wiki kadhaa tu baada ya kutokea mgogoro wa kisiasa nchini humo Juni 2016. Watu wa eneo hilo, hususan waliopoteza makazi na wenyeji wao, walikosa misaada , na miezi iliofuata, watu walilazimika kutorokea maeneo ya ndani zaidi hasa misituni kutokana na hali ya usalama kuvurugika.
Afisa wa afya wa shirika la IOM anaekaa Wau, Dkt Mary Alai, ameeleza kuwa ingawa baadhi ya familia zimeanza kurejea nyumbani kwao lakini watu wanaokadiriwa kufika 40,500 baado wako katika vituo vya walikohama makazi yao mjini Wau pamoja na maeneo mengine ya mbali.