Hatimaye uwanja wa Ndege Puntland wafunguliwa: IOM
Ukarabati kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa jimbo la Puntland- Somalia umekamilika kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM na sasa umeanza tena kufanya kazi baada ya kufungwa kwa kipindi cha miaka kumi na mitano iliopita. John Kibego anatupa maelezo zaidi
(TAARIFA YA JOHN KIBEGO)
Uwanja huo unapatikana katika mji mkuu wa jimbo hilo -Garowe. Utawala wa Puntland ndio uliongoza shughuli za kuukarabati huku shirika la uhamiaji la IOM likipiga jeki juhudi hizo kwa ushirikiano wa serikali kuu ya Somalia pamoja na wadau wengine wa kimataifa.
Katika sherehe ya ufunguzi wa uwanja huo mkuu wa shirika la IOM ofisi ya Somalia , Dyane Epstein, amesema, kuwepo kwa uwanja wa ndege unaofanya kazi barabara mjini Garowe ni mmoja ya hatua nzuri kuelekea mustakbala bora wa uhamiaji,kuwezesha kurahisisha shughuli za kuingia na kutoka , sio tu katika jimbo la Puntland lakini pia Somalia nzima kwa ujumla.
Naye naibu waziri wa masula ya safari za ndege pamoja na viwanja katika jimbo hilo, Suad Salah Nurm, ameupongeza ushirikiano uliopo kati ya serikali ya jimbo la Puntland, na serikali kuu ya Somalia pamoja na washirika wao wa kimataifa likiwemo shirika la IOM kwa kufanikisha juhudi za kurejesha upya kazi za uwanja huo wa ndege wa Garowe.
Miongoni mwa waliohudhuria sherehe hiyo iliofanyika wiki hii ni pamoja na vigogo kutoka serikali ya mkoa huo akiwemo rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmajo. Wengine ni wajumbe kutoka Umoja wa Ulaya, Benki ya Dunia, Umoja wa Mataifa na vile vile kutoka serikali za Uturuki na Ethiopia.