Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somaliland na Puntland zungumzeni badala ya kuzozana- Keating

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Michael Keating akihutubia mkutano na waandishi wa habari. Picha: UNSOM

Somaliland na Puntland zungumzeni badala ya kuzozana- Keating

Umoja wa Mataifa umetaka utulivu na mazungumzo kufuatia mapigano kati ya vikosi vya jimbo lililojitangazia uhuru la Somaliland huko Somalia na jimbo jirani la Puntland.

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Michael Keating ametoa wito huo katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yake na viongozi wa Somaliland akiwemo Rais Muse Bihi Abdi kwenye mji mkuu wa Somaliland, Hargeisa.

Huu ulikuwa ni mkutano wa kwanza kabisa kati ya Bwana Keating na RAis Abdi tangu achaguliwe mwaka jana ambapo walijadili vipaumbele vya serikali yake na masuala ya usalama.

(Sauti ya Michael Keating)

“Msimamo wetu ni kujaribu kupunguza mvutano na kuongeza mashauriano haraka iwezekanavyo kati ya pande zote na iwapo kuna kutokuelewana kokote, basi kuwekwe bayana. Lakini kutumbukia kwenye suluhu za kijeshi na ghasia si njia ya kutatua matatizo”

Miongoni mwa mamlaka za ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM ambao Bwana Keating anaongoza ni kusaidia Somaliland iwe na utulivu na mifumo ya kidemokrasia inayozingatia misingi ya utawala bora.

image
Bwana Keating alipotembelea maeneo ya miamba na mapango ya Laas Geel iliyoko Kaskazini-Mashariki mwa Hargeisa. Picha: UNSOM
Akiwa Somaliland, Bwana Keating alitembelea  pia maeneo ya miamba na mapango ya Laas Geel iliyoko Kaskazini-Mashariki mwa Hargeisa ambako kuna michoro ya kale ya zaidi ya maelfu ya miaka inayoweza kuwa ni kivutio kwa watalii.

(Sauti ya Michael Keating)

“Moja ya sababu iliyonifanya nije hapa ni kwamba ingawa taswira ya eneo hili duniani ni mizozo na majanga, bado ni moja ya kitovu cha ustaarabu. Kwa hiyo wakati ni rasilimali kwa dunia, ni muhimu pia kwa wasomali kutambua kuwa wanaishi kwenye ardhi yenye historia na tamaduni na hii inabadili mwelekeo.”

image
Bwana Keating alipotembelea maeneo ya miamba na mapango ya Laas Geel iliyoko Kaskazini-Mashariki mwa Hargeisa. Picha: UNSOM