Umoja wa Mataifa wampongeza George Weah

30 Disemba 2017

George Weah, ameshinda kiti cha urais nchini Liberia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amemtumia salamu za pongezi na kuahidi kushirikiana naye katika kuimarisha amani na maendeleo.

Ushindi wa Bwana Weah ambaye ni mwanasoka nguli mstaafu wa kimataifa, umetangazwa leo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Liberia kufuatia duru ya pili ya uchaguzi iliyofanyika Jumanne ya wiki hii.

Bwana Guterres kupitia msemaji wake amempongeza pia makamu wa Rais wa Liberia Joseph Boakai kwa kukubali kushindwa kwenye uchaguzi huo.

Halikadhalika amepongeza wananchi wa Liberia kwa kukamilisha mchakato wa uchaguzi kwa amani, pongezi ambazo pia amezielekeza kwa waangalizi wa uchaguzi wa kitaifa, kikanda na kimataifa.

Bwana Guterres amesema hitimisho hilo la uchaguzi kwa amani ni kiashiria kuwa wananchi wa Liberia wako tayari kusonga mbele na kuendeleza amani ya kudumu, utulivu na maendeleo.

Hata hivyo amesema bado kuna changamoto na hivyo umoja ni muhimu baina ya rais mteule, serikali yake na wadau wa kisiasa.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter