Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya raia 5,000 wakimbia DRC wakati wa msimu wa Krismasi

Wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakivuka ziwa Albert kuelekea Uganda.

Zaidi ya raia 5,000 wakimbia DRC wakati wa msimu wa Krismasi

Kutoka Uganda ripoti yaeleza kwamba zaidi ya raia 5,000 wamekimbia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC,  na kusaka hifadhi nchini Uganda tangu tarehe 18 mwezi huu wa Disemba, kufuatia ongezeko la mashambulizi. Maelezo zaidi na mwandishi wetu John Kibego.

(Taarifa ya John Kibego)

Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Uganda, Roco Nuri, amesema zaidi ya elfu nne wamekimbia jimbo la Ituri na kuingia Uganda kupitia Ziwa Albert.

Wengine zaidi ya elfu moja wamekimbia Jimbo la Kivu Kaskazini na kuingia Uganda kupitia vichakani na mipaka ambayo kawaida hutumiwa na wakimbizi, wakidai ongezeko la mashambulio ya vikundi vya wanamgambo.

Bwana Nuri amesema, wanashirikiana na serikali ya Uganda na wadau wengine kuanzisha mapokezi mapya ya wakimbizi na kufungua mapokezi yaliokuwa yamefungwa.

Kumeripotiwa vurugu za kikabila zinazohusisha jamii za Wagegere, Walendu na Wahema ambapo vijiji zaidi ya ishirini tayari vimekimbiwa.

Ripoti ya UNHCR inasema kuwa watu zaidi ya 53,000 wamekimbia DRC, na kusaka hifadhi huku Uganda tangu Januari mwaka huu.