Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sikukuu ya noeli yasherekewa kiaina yake Juba

Wakimbizi wa ndani kwenye mji wa Juba nchini Sudan Kusini wakiwa katika ibada ya Krismasi. (Picha:UNMISS)

Sikukuu ya noeli yasherekewa kiaina yake Juba

Sikukuu ya krismasi imesherehekewa kwa aina yake katika kambi ya wakimbizi wa ndani mjini Juba nchini Sudan kusini kwa hali ya yakupendeza.

Shamrashamra ziliambatana na vijana kwa wazee wakiwa wamevalia nguo za kupendeza, miwani ya jua, nywele zikiwa zimesukwa vizuri na nyuso zao zikionekana na furaha, watoto nao wakiwa wanacheza na wanasesere huku wakielekea kanisani kwa ajili ya ibada maalum, ikiwa ni ishara ya sikukuu katika eneo hili lililogubikwa na vita visivyoisha.

Tumechoka na vita, tunataka hali hii iendelee kila siku isiwe leo amani kesho machafuko, tumeshapoteza ndugu na marafiki wengi, mimi nimekaa hapa miaka minne sasa nataka amani hii na utulivu udumu ili niweze kurejea nyumbani, alisema Makuar Mangan Kohna  mmoja wa wakimbizi wa ndani katika kambi hiyo.

Naye Kamishna Msaidizi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS Unaisi Vuniwaqa, mara baada ya ibada aliwashukuru wakimbizi hao wa ndani kwa kuwapa fursa walinda amani kujumuika nao katika ibada ya sikukuu ya krismasi  na kuwaomba waendelee kuwapatia ushirikiano wakati huu wakiendelea kuwalinda.

image
Walinda amani wa UNMISS kwenye mji wa Juba nchini Sudan Kusini wakijumuika na wananchi ambao ni wakimbizi wa ndani kwenye Ibada ya Krismasi. (Picha:UNMISS)