Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Patia wageni vyakula badala ya kutupa- FAO

Epusha njaa kwa kupika au kupakua kiwango cha chakula unachohitaji. (Picha:FAO/http://www.fao.org/fao-stories/article/en/c/1072865/)

Patia wageni vyakula badala ya kutupa- FAO

Ikiwa nyakati za mwisho wa mwaka ni nyakati za watu kuburudika na kula milo ya aina mbalimbali, shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limetoa wito kwa watu kuwa makini kwa milo wanayoandaa ili waweze kumaliza badala ya kutupa kama njia moja ya kuondokana na njaa. Taarifa zaidi na John Kibego.

(Taarifa ya John Kibego)

FAO imesema inatambua kuwa msimu wa sasa wa sherehe na mapumziko huambatana na milo maalum, mathalani pilau ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki na keki ya ndizi huko Vietnam.

Hata hivyo imesema wakati wa shamrashamra watu huandaa vyakula vingi kupita kiasi na hivyo huishia kwenye mapipa ya taka.

Kwa mantiki hiyo FAO kupitia tovuti yake imetaja mambo sita muhimu ya kuzingatia ili kuepuka au kupunguza utupaji hovyo vyakula kama njia mojawapo ya kutokomeza njaa duniani.

Mosi, usiandae chakula cha watu 50 ilhali wageni ni watano.

Pili mabaki ya vyakula yahifadhiwe kwenye barafu la sivyo wageni wapatiwe ili waende navyo makwao.

Tatu mabaki ya chakula cha usiku, yageuzwe mlo wa asubuhi au mchana kwa siku inayofuatia.

Kadhalika FAO inataka mtu afikirie kwanza kabla ya kuandaa mlo mpya kwa kubadili mabaki ya chakula kuwa mlo.

Tano wageni waruhusiwe kupakua wenyewe chakula ili wachague wanachotaka badala ya kuwajazia wasichopenda.

Na mwisho FAO inasisitiza kuwa kile ambacho mtu hatumii agawie kwa wahitaji badala ya kulundika vyakula asivyotumia.