Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zaidi zachukuliwa dhidi ya DPRK

Jaribio la kombora. (Picha: UM/Maktaba)

Hatua zaidi zachukuliwa dhidi ya DPRK

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja leo limepitisha azimio la kulaani kitendo cha Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK cha kuendelea kufanya majaribio ya makombora licha ya maazimio ya baraza hilo.

Mathalani azimio hilo limesema Korea Kaskazini lilifanya jaribio la kombora la masafa marefu tarehe 28 mwezi uliopita kinyume na maazimio huku nchi hiyo ikiendelea kukiuka masuala mengine muhimu.

Wajumbe kupitia azimio hilo wameenda mbali zaidi na kuelezea wasiwasi wao kuhusu  kitendo cha baadhi ya nchi kuruhusu raia wa Korea Kaskazini kufanya kazi na hivyo kujipatia fedha za kigeni kinyume na kifungu namba 17 cha azimio namba 2375 la mwaka huu wa 2017.

Kifungu hicho kinataka nchi wanachama kuwarejesha makwao raia wa Korea Kaskazini ambao wanafanya kazi na kupata fedha za kigeni.

Kufuatia azimio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepongeza Baraza hilo kwa kuwa kitu kimoja dhidi ya hatua za DPRK.

Bwana Guterres amesema umoja wa aina hiyo ni muhimu katika kufanikisha lengo la kutokomeza silaha za nyuklia na kuweka mazingira ya diplomasia ili kupata amani ya kudumu.