Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali si shwari kwa wasaka hifadhi Ugiriki

UNHCR/S.Baltagiannis
Wahamiaji wanaosaka maisha bora wengine wakinusurika kifo kama mtoto mkimbizi huyu akiwa amepumzika katika kisiwa cha Lesvos huko Ugiriki wakisubiri kufahamu hatma yao ya kuhamishiwa. (Picha: © UNHCR/S.Baltagiannis)

Hali si shwari kwa wasaka hifadhi Ugiriki

Hali si shwari kwenye vituo vya mapokezi na  utambuzi wa wasaka hifadhi kwenye visiwa vya Aegean nchini Ugiriki.

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limesema vituo hivyo ambavyo hutumika kama eneo la mpito kwa wasaka hifadhi kabla ya kuhamishiwa maeneo ya bara ya Ugiriki sasa vimejaa na kutia hofu juu ya usalama wa makundi yaliyo hatarini zaidi kama vile wanawake na watoto.

Msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi, Cécile Pouilly amesema ingawa wameanzisha mbinu mpya ya kuharakisha mchakato wa kuhamisha wahamiaji, bado hali haijatengamaa kwenye visiwa hivyo vya Lesvos, Chios na Samos.

Kwa mantiki hiyo UNHCR inaisihi serikali ya Ugiriki iondoe vikwazo vinavyopoteza muda wakati wa usajili wa wasaka hifadhi.