Filamu ya Háwar yaweka bayana ukatili dhidi ya wayazidi

20 Disemba 2017

Filamu ya Hawar kuhusu mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa jamii ya wayazidi Kaskazini mwa Iraq imeweka bayana ukatili waliofanyiwa watu hao. Tupate taarifa Zaidi na Flora Nducha

(TAARIFA YA FLORA)

Ikiwa imezinduliwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Hawar ikiwa na maana kilio cha msaada imedhihirisha machungu yaliyofuatia mauaji yaliyofanywa na magaidi wa ISIL au Daesh dhidi ya wayazidi wapatao 5000 mwezi Agosti mwaka 2014.

image
Mwanaharakati wa haki za kibinadamu nchini Ujerumani Michael Blum (kushoto) na mwanaharakati wa haki za binadamu, Düzen Tekkal, kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa, kabla ya kuandaa filamu ya Háwar - A Cry For Help. Picha: Matt Wells / UN News Center

Katika mahojiano na idhaa ya Umoja wa Mataifa, Düzen Tekkal ambaye ni muandaaji wa filamu hiyo na alishuhudia mauaji hayo amesema…(Sauti ya Düzen Tekkal)

“Hali ilikuwa si ya kiutu, vitendo vya kikatili walivyofanyiwa wayazidi na ISIL huwezi amini kwamba binadamu anaweza kumfanyia binadamu mwezake. Hapa tunaongelea utumwa, na vitendo visivyo vya kiutu kama ubakaji kwa wanawake na watoto, tunaongelea kufanyiwa ukatili mbele ya ndugu zako. Nikiwa ni muandaa filamu nilichukua jukumu la kupaza sauti na kuongelea janga hili  kwa mataifa mbalimbali ili watu waweze kujua kwamba hii sio ukatili kwa wayazidi tu bali kwa binadamu.”

Naye Michael Blum [BLUMA] ambaye ni  Mkurugezni wa shirika la kiraia nchini Ujerumani lililosaidia kuokoa zaidi ya  wanawake na watoto 1000 wa kiyazidi wakati wa mauaji hayo amesema.. 

(Sauti ya Michael Blum)

“Wakati ISIL walipovamia vijiji vya wayazidi mwaka 2014, ujumbe wa wayazidi waishio Ujerumani ulimuendea mkuu wa mkoa wa Baden-Württemberg  wakiomba msaada.  Mkuu huyo akatuuliza je tufanye nini , tunajua hatuna jeshi la mkoa, basi baada ya kusoma sheria ya mkoa tukakuta kwamba kuna sheria inayoruhusu   misaada ya kibinadamu. Ndipo tulipoamua kuanzisha jitihada za kuwaokoa wanawake elfu moja na kuwaleta   katika mkoa  Baden-Württemberg na wengine 100 katika mkoa wa mwingine.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter