Mtoto 1 kati ya 3 wanatumia inteneti, lazima walindwe:UNICEF:
Wakati fursa ya matumizi ya mtandao wa intaneti ikiongezeka ni lazima dunia hii ya kidijitali iyafanye matumizi hayo kuwa salama kwa watoto ili yaweze kunufaisha hasa wale walio katika hatari zaidi.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF iliyotolewa leo ambayo inaonyesha mgawanyiko wa kidijitali unaochunguza mjadala wa sasa kuhusu athari za mtandao na vyombo vya habari vya kijamii kwa usalama na ustawi wa watoto.
UNICEF inasema licha ya uwepo mkubwa wa watoto mtandaoni huku mtumiaji 1 kati ya 3 wa intaneti duniani kote akiwa ni mtoto, ni hatua kidogo sana zilizochukuliwa kuwalinda watoto kutokana na hatari zake na kuongeza fursa yao ya kupata maudhui salama ya mtandao.
Ripoti inasema serikali na sekta binafsi hazizingatii kasi ya mabadiliko, hivyo zinawaweka watotokatika hatari mpya na kuwaharibu huku zikiwaacha nyuma mamilioni ya watoto wasiojiweza.
Anthony Lake mkurugenzi mkuu wa UNICEF amesema “kwa uzuri na ubaya, teknolojia ya kidijitali sasa ni ukweli usiogeuzwa wa maisha yetu,ulio na changamoto kuu mbili,jinsi gani ya kupunguza madhara na wakati huohuo kuongeza faida za mtandao kwa kila mtoto."