Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hebu fikiria maisha bila maji , kwa watoto wa Yemen hiyo ni kama ada

UNICEF kwa kushirikiana na Benki ya Dunia katika juhudi za kusaidia serikali ya Yemen kuimarisha mfumo wa maji na usafi ili kuzuia Cholera. Picha: UNICEF

Hebu fikiria maisha bila maji , kwa watoto wa Yemen hiyo ni kama ada

Ugonjwa wa kipindupindu na kuharisha umeongezeka mara dufu nchini Yemen mbali na zahma nyingine kama njaa, ukosefu wa mahitaji muhimu na mahangaiko ya vita kila uchao.

Mlipuko huo unatokana na uhaba mkubwa wa maji safi na salama vimesababishwa na kupanda kwa gharama za petroli nchini humo.

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto UNICEF  Geert Cappelaere amesema  wanatoa lita 450, 000  za mafuta kila mwezi lakini kutokana na bei kuongezeka mara mbili zaidi ndani ya mwezi mmoja wamejikuta katika wakati mgumu.

Cappelaere ameongeza kuwa watoto nchini Yemen wameshateseka sana na kwa  muda mrefu , sasa vikwazo vya kusambaza misaada ya kibinadamu vinatakiwa kuondolewa haraka iwezekanavyo ili kunusuru maisha ya watoto zaidi ya milioni 1 waliopo hatarini kutokana na mlipuko wa magonjwa.