Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Warohingya washikamana licha ya taabu ugenini- ripoti

Wakimbizi wa Rohingya wapatiwa huduma za afya kambini Kutopalong. Picha: UNHCR

Warohingya washikamana licha ya taabu ugenini- ripoti

Licha ya kukabiliwa na shida za kiafya na usalama, mshikamano baina ya wakimbizi wa Rohingya huko Bangladesh umeleta matumaini miongoni mwao. Leah Mushi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Leah)

Ikiwa ni mwezi wa nne sasa tangu warohingya waanza kukimbia Myanmar ili kunusuru uhai wao, tathmini imeonyesha kuwa wameimarisha mtandao baina yao ugenini na hivyo angalau kupata matumaini.

Tathmini mpya ya shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR iliyofanyika kwenye kambi zinazohifadhi wakimbizi hao huko Bangladesh imeonyesha kuwa mshikamano baina  yao umepunguza machungu ya kuwepo ugenini.

Hata hivyo Andrej Mahecic ambaye ni msemaji wa UNHCR Geneva, Uswisi amesema licha ya kuwepo kwa matumaini hayo..

(Sauti ya Andrej Mahecic)

“Wakimbizi waliohojiwa wameeleza wasiwasi kadhaa ikiwemo kujisikia kukosa usalama nyakati za usiku kwa kuzingatia makazi yao ni dhaifu, hakuna mwanaga na huduma za maji safi na salama hazitoshelezi.wanawake na watoto wana hofu kuhusu ukosefu wa malazi na hivyo kulazimika kuoga nje alfajiri. Baadhi ya watoto wanalazimika kutembea umbali mrefu kusaka maji na kuni. Wazazi na watoto wanataka huduma ya elimu iwepo na maeneo salama kwa watoto kucheza.”

Hata hivyo Bwana Mahecic amesema ingawa bado wakimbizi wanaingia Bangladesh kutoka Myanmar, kasi imepungua ikilinganishwa na awali.