Zeid alaani kitendo cha Israel kumpiga risasi na kumuua mtu aliyekuwa kwenye kitimwendo

19 Disemba 2017

Nimestaajabishwa sana na kitendo cha jeshi la Israel kumuua kwa kumpiga risasi mtu mwenye ulemavu aliyekuwa anaelekea msikitini siku ya Ijumaa.

Hiyo ni kauli ya Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein kufuatia ripoti ya kwamba mtu huyo Ibrahim Abu Thurayeh aliuawa akiwa kwenye kitimwendo chake.

Ibrahim alikuwa miongoni mwa mamia ya wapalestina walioandamana Ijumaa karibu na uzio kati ya Ukanda wa Gaza na Israel, wakipinga hatua ya Marekani kutambua Yerusalem kuwa makao makuu ya Israel.

Bwana Zeid amesema taarifa zinadhihirisha kuwa jeshi la Israel lilitumia nguvu nyingi kupita kiasi kitendo ambacho ni kinyume na sheria za kimataifa za kibinadamu.

Rupert Colville ambaye ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu huko Geneva, Uswisi amesema ingawa yaelezwa Israel imechunguza kisa hiki..

(Sauti ya Rupert)

“Kamishna Mkuu anatoa wito kwa Israel kuanza mara moja uchunguzi huru na usioegemea upande wowote kuhusu kisa hiki na visa vingine vyote ambavyo vimesababisha majeruhi au vifo, kwa lengo la kuwafikisha wahusika mbele ya sheria kwa uhalifu waliotenda.”

Hili ni janga la pili kumkuta Ibrahim ambapo mwaka 2008 makombora yaliyorushwa na Israel yalisababisha miguu yake miwili kukatika.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter