Wafanyakazi sita wa misaada watoweka Sudan kusini hofu yatanda: OCHA

19 Disemba 2017

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, Alain Noudéhou ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu kutoweka kwa wafanyakazi sita wa misaada ya kibinadamu siku ya Jumapili Decsemba 17, wakiwa barabarani kati ya Wau na Raja kwenye jimbo la Magharibi la Bahr el Ghazal.

Wahudumu hao sita ni pamoja na mfanyakazi mmoja wa kimataifa na watano raia wa Sudan Kusini wanaofanya kazi na mashirika mawili ya kimataifa na moja la kitaifa ya kutoa misaada ya kibinadamu na walitoweka walipokuwa wakisafiri kwenda kugawa misaada.

Kwa mujibu wa shirika la kuratibu misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa OCHA , kuna ripoti zisemazo kulikuwa na mapigano wakati tukio la kutoweka kwao.

Wafanyakazi hao na mashirika yao walikuwa wamekuwa wakitekeleza mkakati wa kuhakikisha uhakika wa chakula, kuokoa maisha, kutoa huduma za afya na lishe katika jimbo Bahr el Ghazal lililoghubikwa na kiwango kikubwa cha utapia mlo Sudan Kusini.

OCHA imetoa wito wa kurejea wakiwa salama wafanyakazi hao na kuzitaka pande zote katika mzozo nchini humo kuheshimu haki za binadamu na mchango wa kuokoa maisha unaotolewa na wafakazi wa misaada.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter