Mwaka wa tano sasa, hali ya watoto bado kintendawili Sudan Kusini- UNICEF

15 Disemba 2017

Ripoti ya shirika la watoto duniani UNCEF imesema Sudan kusini ni moja ya nchini ambako nusu ya idadi ya watoto wameathiriwa na utapiamlo, magonjwa mbalimbali na pia ukosefu wa elimu. Patrick Newman na ripoti kamili.

(Taarifa ya Patrick)

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto wengi Sudan kusini hufanyiwa vitendo vya kikatili, hulazimishwa kujiunga na makundi ya wanamgambo kwa ajili ya kupigana vita na hivyo kuifanya  idadi ya watoto wenye umri wa miaka 13 na kuendelea kuondoka majumbani kwao kufikia milioni 2.4.

Leila Pakkala ambaye ni mkurugenzi wa UNICEF ukanda wa Afrika  mashariki na  magharibi  amesema, hakuna mtoto anayepaswa kupitia suluba ya namna hiyo popote pale duniani.

Akaongeza kuwa watoto wa Sudan kusini wanahitaji mazingira salama na yenye amani wakati huu ambapo vita nchini  humo inaingia mwaka wa tano.

Naye Tim Irwin ambaye ni afisa habari wa UNICEF amehojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa na kusema vita ni kikwazo kwa wahudumu wa misaada kufikia watoto akisema..

(Sauti ya Tim Irwin)

“Ukweli hali ya usalama ni hatarishi sana hata kwa mashirika yanayotoa misaada ya kibinadamu. Ila kubwa zaidi ni suala la utapiamlo kwa  mamilioni ya watoto na kufanya maisha ya watoto kuwa hatarini.”

UNICEF imekuwa mstari wa mbele kutoa msaada ya hali na mali kwa watoto nchini Sudan kusini tangu mwaka 2013, ikiwemo huduma ya chakula kwa zaidi ya watoto laki 6 wanaokabiliwa na utapiamlo,  na vilevile chanjo kwa watoto zaidi ya milioni 3.3.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter