Kituo cha kupima TB Kibong’oto kuleta nuru kwa wachimbaji madini

14 Disemba 2017

Vumbi vumbi wanalokumbana nalo wachimba madini wadogo limeendelea kuwa mwiba katika afya zao. Nchini Tanzania hususan mkoani Manyara, ushuhuda wa mmoja wa wachimbaji wadogo umeonyesha dhahiri shairi kuwa hatua ni lazima zichukuliwe ili kuepusha nguvu kazi hiyo dhidi ya ugonjwa wa Kifu Kikuu au TB ambao ingawa una tiba bado unaleta kadhia. Ukosefu wa vituo vya uchunguzi na matibabu unasababisha baadhi ya wagonjwa kujikuta wanatibu ugonjwa usio sahihi na hivyo kusababisha usugu wa dawa. Umoja wa Mataifa kupitia malengo yake ya maendeleo endelevu, unatambua umuhimu wa tiba sahihi dhidi ya TB. Ni kwa mantiki hiyo Tanzania hivi karibuni ilizindua kituo cha kwanza na cha kipekee nchini humo cha kutoa huduma za kifua kikuu, UKIMWI na magonjwa yatokanayo na shughuli za uchimbaji madini kwa watanzania kwenye hospitali ya Kibong’oto mkoani Kilimanjaro. Ujenzi unafuatia usaidizi kutoka fuko la kimataifa au Global Fund. Je nini manufaa yake? Ungana na Assumpta Massoi kwenye makala hii.