Seneti Mexico msipitishe muswada wa sheria Mexico: Wataalam

14 Disemba 2017

Muswada wa sheria mpya unaolenga kuvipatia vikosi vya ulinzi nchini Mexico kujikita na kazi za polisi bila  kuwajibika kwa jamii unatia shaka kuhusu haki za binadamu

Hayo yamesemwa na wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu hii leo huko Geneva Uswisi.

Wataalamu hao wamesema muswada huo unaotarajiwa kupitishwa leo na baraza la seneti nchini humo, unatakiwa kupingwa kwa kuzingatia hali ya kiusalama na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Mexico

Wamesema muswada huo haujatoa maelezo ya namna vikosi hivyo vitahakikisha vinazingatia haki za binadamu wakati wakitekeleza majukumu yake ambayo mengi wanaweza kuyaita ya usalama wa taifa hivyo kushindwa kuhojiwa na jamii.

Kama hiyo haitoshi, wahanga wa haki za binadamu, asasi za kiraia, mashirika ya kitaifa na kimataifa ya haki za binadamu hayajashirikishwa katika kuandaa mswada huo.

Hata hivyo wataalamu hao wa haki za binadamu  wa Umoja wa Mataifa wameishukuru serikali ya Mexico kwa kuonesha ushirikiano pindi walipowasiliana nao hivi karibuni kuhusu suala hilo.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter