Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kweli nyumbani ni nyumbani: UNHCR

Binti Fadumo , akiwa kwenye biashara yake ya kuuza batiki mjini Kisimayo Somalia. Amerejea nyumbani na kuanza maisha mapya kwa msaada wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR baada ya kuishi ukimbizi kambini Dadaab nchini Kenya kwa miaka mingi. Picha na UNHCR

Kweli nyumbani ni nyumbani: UNHCR

Wahenga walinena msahau kwao mtumwa, na nyumbani ni nyumbani hata iweje. Kauli hiyo si msemo tena bali ni hali halisi kwa maelfu ya wakimbizi wa Kisomali walioamua kuchukua hatua ya kurejea nyumbani baada ya kuishi kwa miaka mingi kwenye makambi ya wakimbizi ya Dadaab na Kakuma nchini Kenya. Flora Nducha na taarifa kamili.

Natts……

Kisimayu nchini Somalia , akiwa nyumbani anaanda kifungua kinywa Fadumo binti wa miaka 24, ambaye maisha yake yote ameishi ukimbizi nchini Kenya, mwaka mmoja uliopita alikata shauri la kurejea nyumbani ili kujenga upya maisha yake na ya nchi yake.

Na kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu ndoto yake ikatimia, akapatiwa mafunzo ya ujasiriamali na kuanzisha biashara ya kuuza na kutengeneza batiki ambayo sasa imeshamiri na kufungua ukurasa mya wa Maisha yake, inamsaidia yeye na familia yake.

Fadumo ni miongoni mwa wakimbizi 75,000 walioamua kurejea nyumbani Somalia kutoka kwenye kambi za Dadaab na Kakuma, akiwa na matumaini makubwa ya maisha ya baadaye hajutii uamuzi wake

(SAUTI YA FADUMO)

“Nina furaha kubwa sana kwamba tulirejea nchini mwetu. Amani anaanza kurejea taratibu, tumerejea kwa watu wetu, tunaishi kwa uhuru, na hakuna anayekuuliza umetoka wapi.”

Kweli baada ya dhiki ni faraja, UNHCR inasema kuna wakimbizi zaidi ya milioni moja wa Kisomali kote duniani na inawasidia wale walioamua kurejea nyumbani Somalia kwa hiyari kama Fadumo kupitia miradi mbalimbali ya ujasiriliamali inayowawezesha kujitegemea na kujenga upya maisha yao na familia zao.