Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fedha sio tatizo kasi ya hatua zetu ndio tatizo : Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza katika mkutano wa viongozi duniani kote wa “dunia moja” jijini Paris Ufaransa. Picha: UM/Video capture

Fedha sio tatizo kasi ya hatua zetu ndio tatizo : Guterres

Viongozi wa dunia leo wamekusanyika mjini Paris Ufaransa wakijaribu kusaka fedha zaidi ili kuusukuma uchumi wa dunia kuwa unaojali mazingira ikiwa ni miaka miwli kamili tangu kutiwa saini kwa mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tambia nchi kuepuka zahma kubwa zaidi ya ongezeko la joto duniani.

Akizungumza katika mkutano huo  wa “dunia moja” , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema dunia haijafanikiwa kushinda vita vya mabadiliko ya tabia nchi ambayo ndio changamoto kubwa ya wakati huu, ana kwamba makubaliano ya Paris yalikuwa ni ya kuweka msingi tu wa hatua zinazopaswa kuchukuliwa , lakini ni bayana kwamba hatua za kusuakusa haziwezi kuufikisha mkataba huo popote na ushahidi uko bayana

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza katika mkutano wa “dunia moja” Paris. Picha: UM/Video capture
(ANTONIO GUTERRES CUT 1)

“Kila siku, katika kila kanda , kurasa za mbele za magazeti zimetawaliwa na vichwa vihusuvyo majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi-vimbunga, mafuriko, ukame, moto. Mabadiliko ya tabi nchi yanakwenda kasi zaidi ya tunavyokwenda sisi.”

Amesema na hiyo ni changamoto kubwa ya dunia hii, kuwa katika vita vya kuokoa maisha na dunia kwa ujumla, lakini cha msingi ni kwamba ina mshirika muhimu ambaye ni sayansi na teknolojia.

(GUTERRES CUT 2)

“ Kwanza kwa sababu kinachotokea sasa ni kile hasa kilichotabiriwa na sayansi. Pili, maendeleo ya kiteknolojia tayari yamefafanua uongo kwamba kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ni tishio kwa uchumi. Biashara  inayojali mazingira ndio biashara nzuri. Ujumbe ni rahisi: wale ambao wanashindwa kuzingatia uchumi unaojali mazingira wataishi katika mustakhbali wa zahma.”

Amesisitiza hivyo ni muhimu kwa serikali, asasi za kiraia , sekta binafsi na sekta ya fedha kujitoa kimasomaso kufanikisha hilo. Akisema anaelewa fedha zinatakiwa na zitaendelea kuwa kichocheo , kati ya kushinda na kupoteza vita hivi, lakini fedha sio kila kitu na sio tatizo, shida ni jinsi ya kuzitumia na wapi zinakotumika

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihojiwa na World Bank katika mkutano wa “dunia moja” Paris. Picha: UM/Video capture
(ANTONIO GUTERRES CUT 3)

“ Tunahitaji kuganga yajayo, yaliyopita si ndwele, tunahitaji watunga será na benki kuu, masoko ya hisa, hifadhi ya jamii , mashirika na wadau wote wa fedha kushikamana katika uwekezaji unaoendana na hatua za mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo endelevu.”