Mwaka mmoja wa mkataba wa Paris, mafanikio ni dhahiri

11 Disemba 2017

Mkutano wenye lengo la kuchagiza utekelezaji wa mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi utafanyika kesho mjini Paris, Ufaransa, ukienda sambamba na maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kutiwa saini kwa nyaraka hiyo.

Viongozi wa ngazi ya juu watashiriki mkutano huo akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres, Rais wa benki ya Dunia pamoja na mwenyeji wao Rais wa Ufaransa.

Wakati wa mkutano huo, hatua zinazochukuliwa za kufanikisha mkataba huo zitawekwa bayana ikiwemo hatua za nchi kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Mathalani zaidi ya nchi 40 zikiongozwa na India zimeungana hivi karibuni na China na kutia saini ushirika wa kimataifa wa nishati ya jua ambao unalenga kuzalisha nishati ya jua ya kiwango cha GigaWati ,1000 ifikapo mwaka 2030.

Nazo benki za JP Morgan Chase na HSBC zimetangaza kuwekeza jumla ya dola bilioni 300 katika miradi isiyoharibu mazingira.

Tayari nchi 170 zimeridhia mkataba huo na kuwezesha kuanza kutekelezwa ndani ya miezi sita, kitendo kilichovunja rekodi kwa mkataba wa kimataifa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud