Wahusika wa mauaji na ukatili dhidi ya Rohingya lazima wawajibishwe: Zeid
Mkuu wa ofisi ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amelaani vitendo vya kikatili vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu vilivyo pangwa na kutekelezwa dhidi watu wa kabila la Rohingya, nchini Myanmar pamoja na miongo kadhaa ya ubaguzi na mateso kwa watu hao.
Bwana Zeid Ra'ad Al Hussein ameyasema hayo katika kikao maalum cha baraza la haki za binadamu mjini Geneva Uswis wakati wa kujadili mustakabali wa watu wa kabila la Rohingya walioko kaskazini mwa jimbo la Rakhine,kwa lengo la kuokoa maisha ya maelfu ya watu hao dhidi ya mauaji ya kimbari yanaofannywa na vikosi vya serikali pamoja na wanamgambo.
Aidha Bwana Zeid amesema katika ripoti ya watalaam huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uchunguzi wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wati wa Rohingya mashahidi ambao ni waatirika waliripoti vitendo vya udhalimu wa kutisha uliofanywa dhidi yao, ikiwa ni pamoja na kuchoma moto kwa makusudi nyumba zao, mauaji ya kiolela dhidi yao na watoto wao na pia ubakaji dhidi ya wanawake .
Zeid ameongeza kuwa ulimwengu hauwezi kufumbia macho vitendo vya kikatili dhili ya waislamu wa kabila la Rohingya. Lazima waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria haraka iwezekanavyo.