Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria ya kuipa nguvu jeshi Mexico itazidisha machungu- Zeid

Kamisha mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid R'aad Al Hussein. Picha na UM/OHCHR

Sheria ya kuipa nguvu jeshi Mexico itazidisha machungu- Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Ali Hussein amesema pendekezo la sheria ya kulipatia jeshi nchini Mexico jukumu la kisheria la kusimamia usalama linatia wasiwasi mkubwa.

Bwana Zeid amenukuliwa huko Geneva, Uswisi akisema kuwa ingawa anatambua changamoto za kiusalama ambazo Mexico inakabiliana nazo,  bado jeshi la ulinzi kupewa jukumu la polisi linatia hofu.

Amesema zaidi ya muongo mmoja wa jeshi kuendesha shughuli za kipolisi katika vita dhidi ya madawa ya kulevya, haujazaa matunda yoyote huku ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ukiendelea.

Ametaja vitendo vya ukiukwaji kuwa ni pamoja an mauaji kinyume cha sheria, mateso kwa raia na watu kutoweshwa.

Tayari rasimu  hiyo ya sheria imepitishwa kwenye bunge la chini tarehe 30 mwezi uliopita lakini bado kuwasilishwa kwa mjadala kwenye baraza la seneti ili hatimaye ipitishwe.