Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wanaume wa Syria wanalawitiwa na kunyanyaswa :UNHCR

Wakimbizi wanaume wa Syria wanabakwa na kunyanyaswa kingono. Picha: © UNHCR/Dominic Nahr

Wakimbizi wanaume wa Syria wanalawitiwa na kunyanyaswa :UNHCR

Utafiti uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR umebaini kwamba ulawiti, mateso na unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanaume na wavulana huenda ni mkubwa zaidi ndani na nje ya Syria kulivyo ilivyodhaniwa hapo awali.

Waathirika wameeelezea madhila yanayowasimu hususani mahabusu ikiwemo kuvuliwa nguo zote na kuachwa utupu, kuwekwa kizani usiku kucha, kufungwa mikono juu usiku kucha, kuteswa na vifaa vya umeme kwenye sehemu za siri, kupigwa risasi sehemu za siri, kulawitiwa na watu wanaowashikilia, na  hata walipowasihi wasulubishaji wao kuwaonea huruma hawakusikilizwa.

Ripoti ya utafiti huo iliyochapishwa leo inaonyesha kwamba ukatili wa kingono na mateso kwa wanaume na wavulana umetapakaa, na matokeo ya utafiti huo yamepatikana baada ya kukusanya tarifa kutoka kwa makundi mbalimbali wakiwemo wakimbizi 196 nchini Iraq, Lebanon na Jordan.

Watafiti wa UNHCR walipokea maelezo pkutoka kwa wanaume na wavulana wa rika zote wakiwemo watoto wa miaka 10 hadi wanaume wa umri wa miaka 80.

Pia utafiti huo umegundua kwamba wavulana wakimbizi katika nchi wanakopata hifadhi wakabiliwa na ukatili wa kingono kutoka kwa wakimbizi wenzao wanaume na pia wanaume katika jamii wanakohifadhiwa.

Lengo la utafiti huo wa UNHCR ni kutanabaisha ukubwa na madhila hayo yanayowakubwa wakimbizi wanaume na wavulana ili kutafuta njia za kushughulikia tatizo hilo na pia mahitaji ya waathirika.