Skip to main content

Uganda tokomeza ndoa za utotoni upate dola bilioni 3 kwa mwaka

Msichana Aziza, mwenye umri wa miaka 17 akiwa na mimba ya miezi tisa. Picha: UNFPA Tanzania

Uganda tokomeza ndoa za utotoni upate dola bilioni 3 kwa mwaka

Ripoti mpya ya Bendi ya Dunia imebaini kuwa iwapo Uganda itatokomeza ndoa za utotoni ifikapo mwaka 2030, basi itakuwa inajipatia faida ya dola bilioni 3 kwa mwaka.

Kinyume cha hapo, ripoti hiyo inasema Uganda itashuhudia kushuka kwa elimu miongoni mwa watoto wa Kike, ongezeko la idadi ya watu sambamba na athari za kiafya pamoja na ukatili wa kijinsia na umaskini.

Akizungumzia ripoti hiyo Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini Uganda Christina Malmberg Calvo amesema gharama ya ndoa za utotoni si kwa mtoto mwenyewe na mwanae bali pia inapoteza fursa ya jamii na uchumi wa nchi.

Amesema mtoto wa kike akienda shule, idadi ya watu itapungua, fursa za mtoto huyo kuajirika au kujiajiri zinakuwa za juu, halikadhalika umaskini na utegemezi vinapungua.

Ripoti hiyo inasema iwapo hii leo wanawake ambao waliolewa wakiwa watoto wasingalikuwa wameolewa, mapato yao yangalikuwa zaidi ya dola milioni 500.

Kwa mantiki hiyo ripoti hiyo ya 10 ya mwelekeo wa uchumi nchini Uganda inasihi serikali kuwekeza kwa wasichana ili kutokomeza ndoa za umri mdogo.

Nchini Uganda mtoto mmoja wa kike kati ya watatu anaolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.