Usawa wa kijinsia katika ajira kuongeza pato la dunia kwa 26%: Phumzile

Uwezeshaji Wanawake utaboresha uchumi. Picha: UN Women

Usawa wa kijinsia katika ajira kuongeza pato la dunia kwa 26%: Phumzile

Shirika la Umoja wa Mataifa la wanawake UN Women, kwa kushirikiana  na shirika la maendeleo la wananwake NAMA huko Sharjah Falme za kiarabu, wamezindua kongamano la kimataifa  la siku mbili kuanzia leo tarehe 4 hadi 5 desemba.

Lengo la kongamano hilo ni kuhamasisha serikali na asasi za kiraia kuwashirikisha wanawake katika  maendeleo ya kijamii ikiwa ni sehemu ya kampeni ya siku 16 ya kupinga ukatili dhidi ya wananake duniani.

Mgeni rasmi Mrugenzi wa UN Women Phumzile Mlambo-Ngcuka amepongeza juhudi za NAMA  kuandaa kongamano linalowapa wanawake jukwa la kimataifa katika kujenga fursa za biashara kwa wanawake, kushirikiana na makampuni, serikali na wajasiriamali, na pia kujenga  ushirikiano kati ya Falme za kiabu, Afrika Kusini na nchi nyingine.

Bi Phumzile amesema uwezeshaji  kiuchumi kwa wanawake ni muhimu  katika  maisha endelevu na  kiuchumi, akitolea mfano wa  uchunguzi wa hivi karibuni ulioonyesha kama wanawake watapewa  jukumu sawa katika masoko ya ajira na wanaume , pato la uchumi wa dunia litaongezeka kwa  asilimia 26 ambapo ni sawa na kiasi cha dola  trillion 28 ifikapo mwaka 2025.