Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maisha baada ya vita kwa wapiganaji wa zamani CAR :FAO

Wapiganaji wa zamani katika kikao cha mafunzo kwenye mji mkuu wa Bangui, CAR. Mafunzo yanafanyika Bangui katika mikoa ilyoathirika zaidi na vita. Picha: FAO

Maisha baada ya vita kwa wapiganaji wa zamani CAR :FAO

Zaidi ya wapiganaji wa zamani 1000 nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR wamejiunga na mradi unaofadhiliwa na shirika la chakula na kilimo FAO ujulikanao kama “Mradi wa Umoja wa Mataifa” kwa ajili ya upokonyaji silaha, uhamasishaji na ujumuishwaji katika jamii. Selina Jerobon na tarifa zaidi

(TAARIFA YA SELINA)

Kauli mbiu ya mradi huo ni rahisi, “acha kushiriki ghasia, weka silaha chini na mbadala wake utapatiwa msaada wa kuanza maisha mapya.” Washiriki wanapatiwa mafunzo maalumu katika masuala ya ulimaji wa bustani, kilimo cha mbogamboga na matunda, ufugaji wa kuku na nguruwe pamoja na kugawiwa zana, mbegu au vifaranga na mifugo wadogo wa kuanzia.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa FAO nchini CAR Jean-Alexandre Scaglia mradi huu ni hatua muhimu katika kuelekea amani na kurejesha matumaini katika jamii. Ameongeza kuwa waanshuhudia machafuko yakiongezeka na kufikia kiwango cha 2013-2014 hivyo kuyapa chaguo makundi yenye silaha , chaguo la kujitoa katika vita ni suala muafaka.

Mradi huo pia unatoa fursa kubwa ya faida za kifedha kwa wahusika ambapo kwa wastani mtu anaweza kupata kuanzia dola 85 hadi dola 500 kwa mwezi hivyo mbali ya kuchagiza amani mradi unasaidia kuinua uchumi.