Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumakinike ili tulinde mali za kitamaduni kwenye mizozo- Azoulay

Mkurugenzi Mkuu wa shirika Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO Audrey Azoulay. Picha: UM/Rick Bajornas

Tumakinike ili tulinde mali za kitamaduni kwenye mizozo- Azoulay

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limepokea ripoti ya utekelezaji wa azimio lake la ambalo pamoja na mambo mengine linalaani uharibifu na usafirishaji wa mali za kitamaduni kwenye eneo yenye vita, kitendo ambacho kinafanywa na vikundi vya kigaidi.

Akiwasilisha ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO Audrey Azoulay amesema kuna nuru katika ulinzi wa mali hizo.

Amesema baadhi ya nchi zimechukua hatua ikiwemo kuweka kumbukumbu ya mali za utamaduni zilizoporwa, kupatia mafunzo maafisa wa forodha juu ya udhibiti wa uingizaji na uuzaji wa bidhaa hizo nje ya nchi.

Hata hivyo amesema hatua zaidi zahitajika.

(Sauti ya Audrey Azoulay)

"Kati ya maeneo 83 ya urithi wa dunia yaliyo chini ya UNESCO katika ukanda wa nchi za kiarabu, maeneo 17 yako kwenye orodha ya kuharibiwa kutokana na vita. Zaidi ya maeneo 100 yenye urithi wa kitamaduni huko Iraq yameharibiwa. Maeneo yote 6 ya urithi wa kitamaduni huko Syria yameharibiwa sana ikiwemo Palmyra, na mji wa Aleppo ambao ni moja ya miji kongwe zaidi sasa ni gofu tupu.”

Bi. Azoulay amesihi nchi ziimarishe utekelezaji wa azimio hilo ikiwemo kuanzisha hatua zinazoelimisha watoto na vijana kuhusu ulinzi na uhifadhi wa mali za kitamaduni.

Halikadhalika ametoa wito kwa ukusanywaji wa takwimu na kubadilishana taarifa ikiwemo taarifa za njia zinazotumika kusafirisha mali hizo.

Ametumia pia fursa hiyo kupendekeza kuwa walinda amani wapatiwe mafunzo ya ulinzi wa mali za urithi wa kitamaduni