Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP na UNFPA washirikiana kuokoa barubaru Laos

Mashirika mbalimbali waadhimisha siku ya mtoto wa kike nchini Laos (Maktaba). Picha: UNFPA

WFP na UNFPA washirikiana kuokoa barubaru Laos

Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwe lile la mpango wa chakula duniani WFP na lile idadi ya watu ulimwenguni UNFPA yameazimia kushirikiana hii leo  katika suala la kuwekeza katika  maendeleo ya vijana barubaru wa kike nchini Laos.

Ushirikiano huo ni kupitia programu iliyobuniwa ikipatiwa jina la Noi ambaye ni msichana barubaru wa Laos akitumika kuelimisha umuhimu wa kuweka mjadala wa wazi na barurabaru wa kike kama njia ya kukabiliana na changamoto wanazopata kundi hilo nchini humo.

Programu hiyo imeweka malengo hadi mwaka 2030 ikipatiwa jina Mfumo wa Noi 2030, na inatumia sanaa kama vile maigizo  kuhamasisha vijana barubaru hasa wa kike wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 19 kujikita katika elimu nchini Laos.

WFP imeelekeza zaidi ya asilimia 70 ya misaada yake nchini Laos ili kupiga vita tatizo la ndoa za utotoni ambazo zimeshamiri sana nchini humo na  kukatiza ndoto za wasichana za kuendelea na elimu.

Frederika Meijer ambaye ni mwakilishi wa UNFPA nchini Laos amesema ushirikiano kati ya WFP na UNFPA katika programu ya Noi  2030, utasaidia utekelezaji wa malengo ya maeneleo endelevu, SDGs hususan lile la elimu bora kwa wote.