Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za hifadhi ya jamii bado tatizo Afrika na Uarabuni- ILO

Kinamama wasubiri huduma za hifadhi ya jamii. Picha: UNICEF/Pierre Holtz

Huduma za hifadhi ya jamii bado tatizo Afrika na Uarabuni- ILO

Ripoti mpya ya shirika la kazi duniani, ILO imeonyesha kuwa zaidi ya nusu ya wakazi wote duniani hawajajiunga na mfumo wa hifadhi ya jamii.

Ikizinduliwa hii leo huko Geneva, Uswisi, ripoti hiyo imesema idadi hiyo ni watu bilioni 4, jambo linalodhihirisha jinsi pengo hilo la hifadhi ya jamii linakwamisha maendeleo endelevu.

Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy Rider amewaambia waandishi wa habari kuwa ingawa nchi nyingi zimeongeza na kuboresha idadi ya mifuko ya hifadhi ya jamii, bado uwekezaji zaidi na utashi wa kisiasa vyahitajika ili kuongeza idadi ya wanufaika wa huduma hiyo ambayo ni haki ya msingi ya binadamu.

Amesema pindi wananchi wanapokuwa wamejisajili na mifuko ya hifadhi ya jamii, manufaa si kwao wao pekee bali pia kwa serikali zao.

(Sauti ya Guy Rider)

"Kwa mwaka huu 2017, ukosefu wa huduma hii ya hifadhi ya jamii nadhani haipaswi kukubalika kabisa. Hii ina maana kwamba matumizi ya fedha za umma katika kupanua wigo wa huduma hii lazima yaongezwe ili idadi ya wanufaika iongezeke hasa barani Afrika na nchi za uarabuni ambako kuna uwekezaji mdogo zaidi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.”

Ripoti hiyo imeonyesha kwamba waathirika zaidi wako vijijini ambako asilimia 56 ya wakazi wake hawana kabisa huduma za afya kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii.

Mfano wa kuigwa ni kwa baadhi ya nchi ambako serikali zimetatua shida hiyo kwa kuwezesha wafanyakazi walio katika sekta isiyo rasmi kusajili malipo yao ya kodi, na baada ya fedha hizo kusaidia kulipia likizo za uzazi na mafao ya ulemavu.