Wanafamilia wahusika na usafirishaji haramu wa watoto- Ripoti

IOM
Usafirishaji haramu wa watoto. Picha: IOM

Wanafamilia wahusika na usafirishaji haramu wa watoto- Ripoti

Ripoti mpya iliyotolewa hii leo kuhusu usafirishaji haramu wa watoto imebainisha ushiriki wa wanafamilia katika utoroshaji wa watoto.

Ikiwa ni ushirikiano wa shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM na shirika la kiraia la Polaris, ripoti hiyo imesema kiwango cha mwanafamilia kushiriki kumtorosha mtoto ni mara nne zaidi kuliko kwa mtu mzima.

Akizungumzia ripoti hiyo Mkurugenzi Mkuu wa IOM William Swing amesema watoto wa kiume ndio hulaghaiwa zaidi na mwanafamilia na kutumbukizwa katika utumwa wa kisasa ikiwemo utumikishaji wa kingono.

Ripoti inapendekeza hatua kadhaa ikiwemo kusaidia kaya kuweka mipango ya muda mrefu kwa familia zao ikiwemo kupatia suluhu vyanzo vya uhamiaji usio salama.

Halikadhalika watoto na familia zao kuwezeshwa kubaini watu na wanafamilia wanaonyanyasa watoto au wale wanaotaka kuwachukua na kwenda kuwatumikisha.

Ripoti pia inataka kuwepo kwa mifumo ya ulinzi wa watoto ambayo kwayo watoto wenyewe wanaweza kuitumia kusaka ulinzi bila kujali hadhi yao ya uhamiaji.