Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya vifo Mediteranea yavuka 3000- IOM

Wahamiaji wa Syria wakiokolewa kwenye bahari ya Mediteranea. Picha ya UNHCR/A. D’Amato.

Idadi ya vifo Mediteranea yavuka 3000- IOM

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM limesema idadi ya watu wanaokufa maji kwenye bahari ya mediteranea imevuka 3000 mwaka huu pekee na hivyo kuendelea kudhihirisha umuhimu wa kusaka suluhu ya kudumu kwa suala la uhamiaji.

IOM imesema idadi hiyo imefikia mwishoni mwa wiki kufuatia ripoti za kuzama kwa meli nyingine iliyokuwa imebeba wahamiaji kupitia njia inayounganisha Afrika ya Kaskazini na Hispania ambapo baadhi ya ripoti zinadai kuwa wahamiaji 31 walifariki dunia na ikiripotiwa wengine kuliwa na papa.

Hata hivyo msemaij wa IOM Geneva, Uswisi Joel Milliman amesema idadi hiyo inatia matumaini kutokana na kuwa ni chini kuliko mwaka jana kwa kuwa mwaka jana kiwango cha 3000 kilifikiwa mwezi Julai.

Amesema kwa kuzingatia idadi hiyo ya watu zaidi ya 30,000 kufa maji tangu mwezi Januari hadi tarehe 2 mwezi huu, ina maana ni wastani wa watu 10 kila siku.

(Sauti ya Joel Milliman)

“Njia hiyo bado inachangia takribani asilimia 70 au 72 ya jumla ya vifo kwenye bahari ya mediteranea kwa mwaka huu, lakini ni zaidi ya asilimia 90 ya vifo kwa hiyo bado inatia wasiwasi.”