Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kijana wa Yemen ashinda dola 15,000 kwa mbinu ya kulinda mazingira

Mhandisi kijana kutoka Yemen Omer Badokhon ashinda tuzo ya bingwa wa uhifadhi wa mazingira duniani. Picha: UM/Video capture

Kijana wa Yemen ashinda dola 15,000 kwa mbinu ya kulinda mazingira

Mhandisi kijana kutoka Yemen Omer Badokhon leo ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya bingwa wa uhifadhi wa mazingira duniani.

Badokhoni mwenye umri wa miaka 24 ameshinda tuzo hiyo inayotolewa na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa na taasisi ya Covestro kutokana na  ubunifu wake wa mtambo unaozalisha umeme kwa kutumia taka kwenye nchi yake iliyoghubikwa na vita.

Mshindi huyo ambaye ni miongoni mwa mabingwa wa dunia kutoka kanda sita, amesema anapenda sana mazingira na nishati endelevu na ndio maana amejitolea kulinda na kuhifadhi mazingira.

Mtambo aliobuni Badokhoni wa kuzalisha nishati kwa kutumia taka utapunguza kiwango kikubwa cha hewa aina ya Methane ambayo inaharibu tabianchi na pia inachafua hewa majumbani na kusababisha vifo.

Badokhoni pamoja na kujipatia dola 15,000 kwa ushindi huo, pia atapata mafunzo ya kina Ulaya na atashiriki mkutano mkuu wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa huko Nairobi, Kenya mwezi ujao.