Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yahaha kukabili mlipuko wa dondakoo Yemen

Ndege iliyokuwa imebeba shehena ya chanjo dhidi ya dondakoo na pepopunda baada ya kuwasili Sana'a Yemen. (Picha:UNICEF/UN0147212/Madhok)

WHO yahaha kukabili mlipuko wa dondakoo Yemen

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limeanza kusambaza dawa ili kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa dondakoo nchini Yemen.

Mwakilishi wa WHO nchini Yemen Dkt, Nevio Zagaria amesema hatua hiyo ni muhimu ili kuondoa aibu itokanayo na watoto kufariki dunia kwa ugonjwa huo wenye chanjo.

Amesema tayari shehena ya dawa za kutibu ugonjwa huo imewasili baada ya njia za anga, majini na ardhini kufunguliwa kufuatia kufungwa kwa wiki tatu.

Shehena iliyowasili inasaidia kuzuia kuenea zaidi kwa bakteria anayesababisha ugonjwa wa dondakoo kwenye viungo vya ndani vya wagonjwa ambao tayari wana maambukizi.

Dkt. Zagaria wamesihi hatua ya kuruhusu huduma hiyo ya misaada ya kibinadamu iendelee ili kuokoa maisha ya watoto, wanawawake na wazee.

Ugonjwa wa dondakoo unarejea huku ukitiwa hofu kubwa kwenye nchi hiyo inayokabiliwa na vita ambapo kati ya wagonjwa 189 walioripotiwa, 20 wamefariki dunia.

Tayari kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo wa kale imenza ikilenga watoto 300,000 wenye umri wa chini ya miezi 12.

Kampeni zaidi itafanyika mwezi ujao ikilenga watoto milioni 3 na vijana.