Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatima ya watoto milioni 180 mbaya kuliko wazazi wao: UNICEF

Watoto wa shule ya msingi nchini Ghana wacheza wakionyesha furaha na matumaini. Picha: UNICEF Ghana

Hatima ya watoto milioni 180 mbaya kuliko wazazi wao: UNICEF

Licha ya hatua zilizopigwa kimataifa, mtoto 1 kati ya 12 duniani wanaishi katika nchi ambazo matarajio yao leo ni mabaya kuliko ya wazazi wao, kwa mujibu wa tathimini iliyofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwa ajili ya maadhimisho ya siku ya watoto duniani yanayofanyika leo.

Tathimini hiyo inasema watoto milioni 180 wanaishi katika nchi 37 ambako wana hatihati kubwa ya kuishi katika ufukara, kutosoma au kuuawa kikatili kuliko watoto walioishi katika nchi hizo hizo miaka 20 iliyopita.

Mkurugenzi wa takwimu, utafiti na sera wa UNICEF Laurence Chandy anasema wakati kizazi kilichopita kimeshuhudia hatua kubwa katika kupandisha kiwango cha maisha ya watoto duniani, ukweli unasalia kwamba watoto kutoka jamii za walio wachache zilizosahaulika wametengwa katika hatua hizo na sio kosa lao wala la familia zao.

Kwa mujibu wa tathimini hiyo idadi ya watu wanaoishi kwa chini ya dola 1.90 kwa siku imeongezeka katika nchi 14, huku uandikishaji wa watoto wanaoingia shule za msingi ukishuka katika nchi 21 ikiwemo Syria na Tanzania, na vifo miongoni mwa watoto wa chini ya miaka 19 vikiongezeka katika nchi 7 zikijumuisha Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

UNICEF inasema sababu kubwa ni , vita, ugaidi, matatizo ya kiuchumi, kuongezeka kwa idadi ya watu na umasikini.

UNICEF leo inaadhimisha siku ya watoto kwa watoto kote duniani kushika hatamu na majukumu ya watu wazima katika matukio mbalimbali kwenye nchi 130 ili kuwapa jukwaa la kusaidia kuokoa maisha ya watoto, kupigania haki zao, kutoa kilio chao na kuelezea hofu zao.