Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu bunifu ya mawasiliano yampatia tuzo ya Umoja wa Mataifa

Meja Seitebatso Pearl Block , mlinda amani kutoka Afrika Kusini, (kushoto) akitunukiwa tuzo ya mchechemuzi wa mwaka ya Umoja wa Mataifa katika masuala ya jinsia kutoka Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau na Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix. (Picha:UN/Isaac Alebe Avoro Lu'ub)

Mbinu bunifu ya mawasiliano yampatia tuzo ya Umoja wa Mataifa

Mlinda amani kutoka Afrika Kusini, Meja Seitebatso Pearl Block leo ametunukiwa tuzo ya mchechemuzi wa mwaka ya Umoja wa Mataifa katika masuala ya jinsia.

Meja Block ambaye amekuwa anahudumu katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO ameshinda tuzo hiyo baada ya kubuni mbinu rahisi inayoweza kuwafikishia wananchi taarifa muhimu kwa haraka ikiwemo zile za kukabiliana na ukatili wa kijinsia na kingono.

Meja Block amefafanua mbinu hiyo alipohojiwa na kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa, UNIC huko Pretoria, Afrika Kusini.

(Sauti ya Meja Block)

“Una simu yako ya kiganjani na unapokea ujumbe unaokupatia matumaini kuwa kuna mtu anafuatilia, kuna mtu anatambua unachopitia na inakupata namba za mawasiliano nani umpigie simu na wapi uripoti unyanyasaji wa aina hiyo.”

Mfumo huo ambao Meja Block ameweza kubuni baada ya mashauriano na watoa huduma za simu nchini DRC, utazinduliwa kabla ya mwisho wa mwaka huu ambapo amesema..

(Sauti ya Meja Block)

“Ni mbinu yenye gharama nafuu tunayoweza kutumia na inakupatia hakikisho kufikia wananchi mashinani.”

Tuzo hiyo inakabidhiwa leo huko Vancouver, Canada wakati wa mkutano wa mawaziri wa ulinzi kutoka nchi 80 wanachama wa Umoja wa Mataifa.