Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MINUSCA yatoa wito wa utulivu baada ya ajali iliyomuua mwanafunzi Bangui

Logo_MINUSCA

MINUSCA yatoa wito wa utulivu baada ya ajali iliyomuua mwanafunzi Bangui

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA umekaribbisha taarifa ya serikali ya CAR baada ya tukio la ajali ya bahati mbaya  leo asubuhi iliyokatili maisha ya kijana mwanafunzi mjini Bangui.

MINUSCA imesikitishwa na kifo hicho na kuungana na serikali kutoa wito wa kudumisha utulivu miongoni mwa wananchi baada ya tukio hilo kuzusha maanadamano ya ghasia mjini Bangui yanayoulenga Umoja wa Mataifa.

Katika tukio hilo waziri wa habari na msemaji wa serikali ya CAR akaeleza kwamba MINUSCA ingependa kuwafahamisha kuwa gari lililomgonga na kumuua mwanafunzi huyo si mali yake lakini lilikuwa likiendeshwa  na mwanajeshi wa jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati (FACA)

Saa chache baada ya ajali hiyo gari la Umoja wa Mataifa lililokuwa likipita Bangui lilishambuliwa na watu wenye hasira na kuchomwa moto hali iliyohatarisha maisha ya abiria waliokuwemo ambao waliponea chupuchupu.

Pia gari la zimamoto lililotumwa na MINUSCA lilishambuliwa na umati wa watu na kuharibiwa ambapo askari mmoja wa zimamoto alijeruhiwa. Matukio haya mawili kwa mujibu wa MINUSCA yalifuatiwa na mashambulizi mengine kadhaa dhidi ya magari ya mpango huo katika mji mzima wa Bangui na kuashiria kwamba ni machafuko ya kupangwa.

MINUSCA inashirikiana na serikali, jeshi la polisi la nchi hiyo na wadau wengine kuhakikisha utulivu unarejea katika mji huo mkuu wa Bangui.