Mkutano wa kimataifa wa muongo wa watu wa asili ya Afrika wakunja jamvi Geneva

24 Novemba 2017

Kamishna mkuu  wa Haki za binadamu  wa Umoja wa  Mataifa Zeid Ra'ad al  Hussein amekemea unyanyaswaji wa watu wenye asili ya Afrika unaoendelea katika nchi mbalimbali  duniani huku sauti zao zikipuuzwa hata wanapoandika historia zao kwenye vitabu ili dunia iweze kujua yanayowasibu.

Kamishna huyo mkuu  ametoa kauli hiyo leo huko  Geneva nchini Uswisi, katika hotuba yake ya kuhitimisha mkutano wa siku mbili wa kikanda, unaojumuisha watu wenye asili ya Afrika kutoka Bara la Ulaya, Asia ya Kati na Amerika ya Kaskazini wenye lengo la kubadilishana uzoefu, kuangalia changamoto, fursa na maendeleo ya harakati za kuhakikisha maisha ya watu weusi yanaheshimiwa.

Ametolea mfano wa ripoti kadhaa zikionyesha jinsi watu wenye asili ya Afrika wanavyokuwa wakipekuliwa na kushukiwa kwenye matukio mbalimbali na jeshi la polisi huku wakina mama na watoto wakiendelea kupata huduma mbovu za afya.

Kamishna Zeid amesisitiza umuhimu wa kuongea ukweli katika mambo yaliyopita kwakuwa yatasaidia  kujipanga vyema kwa mambo ya sasa na ya wakati ujao katika kuhakikisha haki za watu wote duniani zinaheshimiwa.

Mkutano huo ulioandaliwa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa uliwaleta pamoja nchi wanachama, mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya kikanda, taasisi za kitaifa za haki za binadamu, na asas iza kiraia hususani za watu wenye asili ya Kiafrika katika kanda ya Ulaya, pia wataalamu wa masuala ya haki za binadamu walishiriki katika mijada mbalimbali.