Watu Zaidi ya 230 wauawa kwenye shambulio la kigaidi Misri, UM walaani

24 Novemba 2017

Watu takribani 235 wameuawa na wengine zaidi ya 109 kujeruhiwa kwenye shambulio la kigaidi lililofanyika leo huko Sinai nchini Misri.

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali shambulio hilo la kikatili lililowalenga waumini waliohudhuria swala ya Ijumaa kwenye msikiti wa Al Rawdah mjini Bir al -Abed.

Wajumbe hao wa baraza wametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga hao na serikali ya Misri na kuwatakia nafuu ya haraka majeruhi .

Wajumbe hao wamerejelea kauli kwamba ugaidi katika mfumo wowote ule ni moja ya vitisho vikubwa vya amani na usalama wa kimataifa na kusisitiza haja ya kuwafikisha wahusika kwenye mkono wa sharia wakiwemo watendaji, waandaaji, watoaji wa fedha na wafadhili huku wakiyataka mataifa yote kutimiza wajibu wao chini ya sharia za kimataifa na maazimio ya baraza la usalama kwa kushirikiana na serikali ya Misri na mamlaka zote husika katika jambo hilo.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akipazia sauti yake kulaani shambulio hilo amesema ni lazima waliotekeleza shambulio hilo la kinyama leo wafikishwe mbele ya sheria huku akitoa wito wa mshikamano wa kimataifa kufanikisha azma hiyo.