Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi na wahamiaji watumia njia tofauti kufika Ulaya:UNHCR

Wakimbizi wakiwasili Ulaya kwa njia ya boto kupitia bahari ya Mediterranea. Picha na UNHCR

Wakimbizi na wahamiaji watumia njia tofauti kufika Ulaya:UNHCR

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR inaonyesha mabadiliko katika njia zilizotumiwa na wahamiaji na wakimbizi kuingia Ulaya katika robo ya tatu ya mwaka 2017.

Kwa mujibu wa Pascale Moreau, mkurugenzi wa UNHCR kanda ya Ulaya katika miezi michache iliyopita njia ya bahari kuelekea Ugiriki imekuwa na mvuto mkubwa , huku watu wanaowasili Italia kutumia bahari wamepungua na kushuhudia wahamiaji na wakimbizi wengi wakitumia njia tofauti kuingia barani Ulaya.

Ripoti hiyo inasema idadi ya watu wanaovuka bahari kutoka Libya na kuingia Italia imeshuka, kukiwa na jumla ya watu 21,700 waliowasili Italia kwa njia ya bahari kati ya Julai na Septemba, ikiwa ni idadi ndogo kabisa kwa kipindi kama hiki kwa miaka mine iliyopita.

Ripoti pia inasema idadi kubwa ya watu walioingia Italia mwaka huu walitokea Tunisia, Uturuki na Algeria na raia wa Syria, Morocco na Nigeria ndio walioongoza kwa kuwasili Ulaya kupitia bahari ya Mediterranea.

Kwa mujibu wa UNHCR Ugiriki ndio inayoshuhudia idadi kubwa ya watu wanaowasili kwa njia ya bahari na nchi kavu tangu kuanza kwa majira ya kiangazi na mwezi Septemba wahamiaji na wakimbizi 4,800 waliwasili pwani ya Ugiriki ilikuwa ni idadi kuwa kabisa kwa mwezi mmoja tangu Machi 2016 na wengi wakitokea Syria, Iraq na Afghanistan.

Ripoti ineleza kuwa wanaingia kutoka Uturuki hadi Romania kupitia bahari nyeusi na pia imeainisha madhila yanayowakabili wanawake na wasichana wahanga wa usafirishaji haramu na watoto zaidi ya 15,200 ambao wako peke yao au waliotenganishwa na wazazi wao walipowasili.