Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dawa mseto ya Artemisinin imesaidia kupunguza malariaTanzania:WHO

Kampeni ya kutokomeza malaria kwa kufundisha wananchi matumizi na umuhimu wa vyandarua vyenye dawa nchini Tanzania. Picha na WHO

Dawa mseto ya Artemisinin imesaidia kupunguza malariaTanzania:WHO

Matumizi ya dawa mseto ya Artemisinin au (ACTs) kama chaguo la kwanza la matibabu tangu mwaka 2001 imesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa malaria katika nchi zilizoghubikwa na ugonjwa huo kwa muda mrefu imesema leo ripoti ya ufuatiliaji ya shirika la afya duniani WHO.

Ripoti hiyo inasema mafanikio yamepatika kwa nchi hizo kuchanganya matumizi ya dawa mseto na mbinu zingine kama vyandarua vilivyowekwa dawa, kupuliza dawa majumbani na kufanya vipimo haraka.

Hata hivyo ripoti hiyo ya WHO imeonya kwamba moja ya tishio kubwa la mafanikio hayo ya kudhibiti malaria katika miaka ya karibuni ni usugu wa dawa za kuzuia malaria , hivyo shirika hilo limesisitiza kwamba kulinda ufanisi wa matibabu yaliyopendekezwa ya malaria ni kipaumbele cha juu kwa nchi zinazoathirika na malaria na jamii ya malaria ya kimataifa.

Kwa Tanzania Dr Marina Warsame kutoka program ya kimataifa ya malaria kwenye shirika la WHO na Dr Ritha Njau wa ofisi ya WHO Tanzania wamesema dawa mseto imeanza kutumia Tanzania tangu mwaka 2006 na imeonyesha mafanikio makubwa, kwa mwaliko maalumu wa serikali wataalamu hao wametumia juma zima mkoani Tanga (Novemba 17-22 ) kuendesha uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini ufanisi wa dawa hizo katika maeneo sita , na kutathimini visa 500 kwa kuzingatia misingi yote inayohitajika.

Baada ya uchunguzi huo WHO imepongeza timu husika na kusema uchunguzi kama huo utasaidia na ni muhimu hasa kubaini changamotoza kupambana na malaria kama usugu wa vijiumbe maradhi.