Watoto wa kike warohingya wasimulia walivyokumbwa na ukatili wa kingono

22 Novemba 2017

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linawapatia msaada watoto wa kike na wanawake wa kabila la Rohingya ambao wamekumbwa na vitendo vya ukatili wa kingono wakiwa nchini mwao Myanmar.

(Taarifa ya Assumpta)

Nats..

Watoto hawa wakimbizi kutoka Myamar wakielekea nchi jirani ya Bangladesh baada ya kukumbwa na ukatili nchini mwao Myanmar.

Mmoja wao ni Khadija mwenye umri wa miaka 16 ambaye anasimulia kilichomkuta kabla ya kukimbia.

(Sauti ya Khadija)

 “Nilikuwa nimejificha kwenye zizi la mbuzi na ndipo wanajeshi waliponiona. Wanne hivi au watano walinivuta. Halafu watatu wakaninajisi. Nilipoteza fahamu.”

Khadija anasema baada ya kitendo hicho, yeye na wengine waliokumbwa na visa kama hivyo hawakuweza kufunga jicho kwa hofu..

(Sauti ya Khadija)

 “Nilikuwa naogopa. Hatukuweza kulala usiku kucha kwani tulihofia watarudi tena. Ndio maana tulikimbia. Walibaka na kutesa wanawake na watoto wa kike kila wakati.”

Hivi sasa Khadija na wenzake wanaishi kwenye kambi ambako shirika la Umoja wa Mataifa limeweka maeneo salama kwa wasichana barubaru ili waweze kuzungumza, kubadilishana mawazo na kupata ushauri nasaha na usaidizi ili wakabili mazingira magumu waliyopitia.