Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan wekeni mazingira bora wakimbizi warejee Darfur- Ripoti

Wakimbizi wa ndani wa Sudan wanasajiliwa na maafisa wa WFP Darfur. Picha: WFP

Sudan wekeni mazingira bora wakimbizi warejee Darfur- Ripoti

Serikali ya Sudan imetakiwa kutunga sera thabiti na za uwazi za kuwezesha wakimbizi wa ndani wapatao milioni 2.6 huko Darfur waweze kurejea nyumbani kwa hiari na kujumuika mpya katika jamii.

Wito huo umo kwenye ripoti mpya ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa na ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika huko, Darfur, UNAMID.

Ripoti hiyo imesema licha ya makubaliano ya mwezi Juni mwaka 2016 ya sitisho la mapigano kati ya serikali ya Sudan na vikundi kadhaa vilivyojihami, bado ukatili dhidi ya wakimbizi wa ndani umeendelea na watekelezaji wanakwepa sheria.

Msemaji wa ofisi hiyo ya haki za binadamu Rupert Colville amemnukuu Kamishna Mkuu wa haki za  binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein akitaka masuala ya kimsingi yanayozuia wakimbizi hao kurejea nyumbani.

Mambo hayo ni pamoja na ukosefu wa huduma za msingi na mapigano kutoka kwa wanamgambo.