Licha ya usalama duni, makusanyo ya mapato Afghanistan yaongezeka

21 Novemba 2017

Benki ya Dunia imepongeza jinsi ambavyo Afghanistan imechukua hatua kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Katika ripoti yake ya mwaka  huu, benki hiyo imesema katika miezi nane ya kwanza ya mwaka huu ukusanyaji mapato umeongezeka kwa asilimia 13.

Hata hivyo mwakilishi mkazi wa Benki ya Dunia nchini Afghanistan Shubham Chaundri ameangazia kasi ya ukuaji uchumi akisema ni kidogo kwa uchumi umekua kutoka asilimia 2.2 mwaka jana hadi asilimia 2.6 mwaka huu.

Amesema kiwango hicho kidogo cha ukuaji wa asilimia 0.4 kinatokana na kuendelea kudorora kwa usalama na hivyo wafanyabiashara kutokuwa na imani ya kuwekeza.

Bwana Chaundri amesema usalama unadorora kila uchao na hali imezidi kutwama tangu vikosi vya ulinzi vya kigeni vianze kuondoka nchini humo mwaka 2014.

Hata hivyo amepongeza hatua za serikali za kuazimia kuna amani na usalama nchini kote akisema huo ndio msingi wa maendeleo.

Ukuaji uchumi Afghanistan unatarajiwa kufikia asilimia 3.2 mwakani iwapo hali ya usalama haitadorora zaidi.