Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM nayo yapaza sauti dhidi ya bishara ya utumwa kwa wahamiaji Libya

Mkurugenzi Mkuu wa IOM William Lacy Swing akizungumza na Christiane Amanpour, CNN kuhusu utumwa wa uhamiaji nchini Libya. Picha: IOM

IOM nayo yapaza sauti dhidi ya bishara ya utumwa kwa wahamiaji Libya

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limekaribisha wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wa kutaka biashara ya utumwa kwa wahamiaji nchini Libya ikomeshwe na uchunguzi wa kina ufanywe baada ya ripoti na picha za video kuonyesha wahamiaji Waafrika nchini Libya wanauzwa kama watumwa.

Mkurugenzi mkuu wa IOM bwana William Lacy Swing amesema shirika hilo linashirikiana na malaka nchini Libya kwa ajili ya kutaka kukomesha usafirishaji haramu wa binadamu na kutoa msaada kwa waathirika.

Ameongeza kuwa kuna mapendekezo kadhaa yaliyotolewa na IOM ambayo linataka serikali ya Libya iyatilie maanani, kwanza ni kutoharamisha wahamiaji na wakati huohuo kufanya utumwa na mifumo mingine ya unyanyasaji kuwa ni uhalifu unaostahili adhabu kali, pili kuipa serikali ya Libya uwezo wa kiufundi na mafunzo ya kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na suala la utumwa, tatu kubadili vituo vya kizuizi kwa wahamiaji kuwa vituo vya wazi vya mapokezi na nne kuruhusu IOM na wadau wengine kuchukua jukumu la malazi, chakula na huduma za matibabu kwa wahamiaji wanaorejeshwa na walinzi wa pwani wa Libya ili wasiangukie mikonini mwa wasafirishaji haramu.

Bwana Swing amesisitiza kuwa ili kukomesha bishara hiyo ya utumwa ni lazima kukomesha kwanza usafirishaji haramu.