Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zahitajika kuimarisha huduma za kujisafi kwa warohingya

Watoto wanawa mikono kando ya mto huku wakimbizi wengine wakikusanyika kwenye kituo cha usajili. Picha; UNICEF

Hatua zahitajika kuimarisha huduma za kujisafi kwa warohingya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF lina wasiwasi mkubwa juu ya ripoti ya kwamba wakimbizi wa Rohingya huko Bangladesh wako hatarini kukumbwa na magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo safi na salama kutoka visima vilivyo eneo la Cox’s Bazar.

Takwimu za shirika la afya ulimwenguni WHO, zinaonyesha kuwa maji kwenye eneo hilo yana vimelea vya bakteria kwa asilimia 62 na hivyo kuwaweka wakimbizi hatarini kuambukizwa magonjwa ya tumbo kama vile kuhara.

Hadi sasa watu 10 wamefariki dunia kati ya wagonjwa zaidi ya elfy 36 walioripotiwa kati ya Agosti hadi tarehe 11 mwezi huu na UNICEF inasema iaddi ya wagonjwa inazidi kuongezeka.

Christophe Boulierac, msemaji wa UNICEF, Geneva, Uswisi anaeleza chanzo cha maji hayo kuwa na vijijidudu.

(sauti ya Christophe)

“Baadhi ya mabomba ya visima ndani ya kambi hayakuchimbiwa chini vya kutosha na yamesongamana na hivyo ni vigumu kuzuia vijidudu vya bakteria kupenya. Halikadhalika maambukizi yanaweza kusababishwa na tabia za uchafu kama vile matumizi ya kontena chafu au tabia za watu katika kutumia maji.”

Hivi sasa UNICEF inashirikiana na mamlaka kuchunguza kiwango cha uchafuzi kwenye maji na kuhakikisha ujenzi wa mabomba unakidhi viwango vya kimataifa.