UM wachukizwa na ripoti za waafrika kuuzwa kama watumwa Libya
Kufuatia habari ya kwamba wahamiaji wa Afrika walioko nchini Libya wanauzwa kama watumwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa na kueleza kushtushwa kwake na kitendo hicho.
(Sauti ya Guterres)
“Nimeshtushwa na habari na video vinavyoonyesha wahamiaji wa Afrika wakiripotiwa kuuzwa kama watumwa.”
Hivyo akasema..
(Sauti ya Guterres)
“Nachukizwa na vitendo hivi vya kusikitisha natoa wito kwa mamlaka zote zenye uwezo kuchunguza shughuli hizi kwa kina bila kuchelewa na kuwafikisha watekelezaji wa vitendo hivi mbele ya sheria.”
(Sauti ya Guterres)
“Utumwa hauna fursa katika dunia yetu. Na vitendo hivi ni miongoni mwa vitendo vya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na vinaweza kuwa uhalifu dhidi ya binadamu.”
Katibu Mkuu amesihi nchi zote kusaini na kuridhia mkataba wa kimataifa dhidi ya uhalifu unaovuka mipaka pamoja na itifaki zake huku akisihi nchi ziungane kupinga kitendo hicho na kuimarisha uhamiaji halali.