Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa mara ya tatu baraza la usalama lashindwa kuongeza muda wa JIM:

Wajumbe wa baraza la usalama wakipiga kura kuhusu mswada wa kuongeza muda wa JIM. Picha na UM/Kim Haunghtoun

Kwa mara ya tatu baraza la usalama lashindwa kuongeza muda wa JIM:

Kwa mara ya tatu ndani ya siku mbili baraza la usalama la Umoja wa Mataifa Ijumaa limeshindwa kupitisha azimio la jukumu la jopo la kimataifa linalochunguza matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria kutokana kwa sababu ya kura ya turufu ya Urusi nchi ambayo ni mjumbe wa kudumu wa baraza hilo.

Jukumu la shirika la pamoja la kupinga matumizi ya silaha za kemikali (OPCW)-na jopo la Umoja la Umoja wa Mataifa la mkakati wa pamoja wa uchunguzi (JIM) linamaliza muda wake hii leo.

Endapo azimio lililowasilishwa na Japan lingepitishwa muda wa JIM ungeongezwa kwa kipindi cha siku 30 na kuwa na fursa ya muda huo kuongezwa zaidi na baraza la usalama endapo ingehitajika.

Mbali ya Urusi , Bolvia ilipiga kura ya kupinga mswada huo, mjumbe mwingine wa kudumu Uchina hakupiga kura. Kura ya kupinga au ya turufu kutoka kwa mmoja kati ya wajumbe watano wa kudumu wa baraza la usalama ( Uchina, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani ) inamaanisha azimio haliwezi kupitishwa.

Jana miswaada miwili ya azimio kuhusu JIM, moja lililodhaminiwa na Marekani na mwingine na Bolvia ilishindwa kupita kwenye kikao cha baraza la usalama cha wajumbe 15.

JIM ilianzishwa mwaka 2015 na baraza la usalama ili kubaini watu, mashirika, vikundi au serikali zinazotekeleza, kuandaa, kufadhili au kujihusisha na matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria.